Hesperian Health Guides

Badilisha mitazamo juu ya uzazi wa mpango

Katika sura hii:

Mara nyingi, mpango kazi utajumuisha shughuli za kubadilisha fikra hasi juu ya uzazi wa mpango. Hi ni muhimu hasa panapokuwepo vikwazo vya kisiasa, fikra zisizo na uhakika, na sababu za kiutamaduni au kidini ambazo zinachangia huduma za uzazi wa mpango kutopatikana kwa kila mwanamke.

Pambana na fikra zisizo na uhakika

Fikra potovu nyingi juu ya uzazi wa mpango zinatokana na maneno ya mitaani au imani zisizo za ukweli juu ya uzazi wa mpango. Usambazaji taarifa sahihi juu ya njia tofauti za kuzuia mimba husaidia watu kufikiria manufaa ya uzazi wa mpango. Taarifa zilizomo katika sura hii zinaweza kusaidia kupunguza tatizo hili.

Nani ana nguvu za kushawishi?

Mitazamo na mawazo tofauti ya kisiasa vinaweza kuingilia haki ya wanawake kupanga familia zao na kuzuia mimba zisizotarajiwa. Zoezi lifuatalo, ambalo ni igizo dhima, linaweza kutumika kuangalia kwa karibu zaidi nani hasa ana nguvu ya kushawishi uchaguzi wa wanawake wa njia za kuzuia mimba. Unaweza pia kutumia zoezi hili kuchochea mjadala, kuibua maswali juu ya mitazamo tofauti juu ya afya ya uzazi, na kujadili jinsi gani ya kukabiliana ipasavyo au kupambana na mitazamo hasi.

Zoezi Igizo dhima juu ya mjadala wa uzazi wa mpango

  1. Andaa orodha ya vikwazo vya kisiasa kuhusiana na uzazi wa mpango, na orodha ya mitazamo na imani ambazo zinaweza kuchangia au kukwaza upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango kwa wanawake wote. Chagua vikwazo 3 hadi 5 kutoka kwenye orodha hizi kutumia kwenye igizo dhima.
  2. Waombe watu 3 hadi 5 kuigiza nafasi za watu wenye mitazamo mahsusi ya kuunga mkono au kupinga uzazi wa mpango. Waeleze waigizaji kwamba wajibu wao siyo kuigiza watu halisi ila kuongea kama mtu kutoka kikundi au taasisi mahsusi ambayo inahimiza mtazamo fulani. Wambie washiriki kukaa au kusimama kwenye mstari na kutambua kila mtu kwa lebo aliyowekewa.
  3. Omba watu 2 au 3 kuigiza nafasi za waandishi wa habari ambao wataliuliza maswali jopo la wanakikundi juu ya uzazi wa mpango. Andaa maswali kwa kushirikiana na ‘waandishi wa habari‘ kabla ya igizo kuanza.
  1. Wezesha ‘waandishi wa habari’ kwa zamu kuanza zoezi kwa kuuliza maswali yaliyoandaliwa.
    Swali kutoka kwa mwandishi wa habari litajibiwa na watu 3 ambao wamebandika alama ya "mkuu wa kiwanda," "mkuu wa shule," and "kiongozi wa dini."
    Kwa nini serikali igharamie kliniki za huduma za uzazi wa mpango nchini?
    Huwa tunapoteza fedha kila mara mfanyakazi anapopunguza uzalishaji kwa sababu ya ujauzito. Anapoamua kuacha kazi, tunazalimika kutafuta mwingine ambaye naye huhitaji muda ili kufundishwa kazi.
    Kuwaelimisha vijana juu ya ujinsia na uzazi wa mpango huwafanya kuwajibika zaidi. Sitaki wanafunzi watakaoacha shule kwa sababu ya ujauzito.
    Watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu! Kwa maoni yangu, serikali haipaswi kujihusisha na mambo ya uzazi wa mpango.
  2. Toa fursa kwa watazamaji kuuliza maswali au kutoa maoni kwa jopo.
  3. Baada ya igizo dhima, wezesha waigizaji wote kuondoa lebo zao na kurudi kwenye kikundi kikubwa. Wambie wanakikundi kutafakari juu ya zoezi zima. Yafuatayo ni baadhi ya maswali ambayo unaweza kutumia kuongoza mjadala:
    • Ni mitazamo gani ambayo inaunga mkono uzazi wa mpango kwa baadhi ya wanawake tu? Ni wanawake gani ambao wameachwa nje? Kwa nini?
    • Ni mitazamo gani ambayo inaweka mahitaji ya wanawake kwanza? Je mitazamo hiyo inachangia au kukwaza namna gani uwezo wa wanawake kufanya maamuzi yao juu ya matumizi ya njia za uzazi wa mpango?
    • Tunawezaje kukabiliana na mawazo yanayohoji au kupinga uzazi wa mpango?
    • Kwa kutumia mawazo mapya katika sura hii, tuchukue hatua gani za kuleta mabadiliko?

Tafuta viongozi ambao wanaweza kusaidia kusukuma mbele juhudi za kukuza uzazi wa mpango

Fanya zoezi la kutambua viongozi wenye nguvu (kinaandaliwa) ambao wanaweza kusaidia kushinikiza mitazamo chanya juu ya uzazi wa mpango na upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango. Tafuta watu wengine na taasisi za kusaidia uzazi wa mpango, na pia njia za kufanya kazi pamoja na wadau wengine wa uzazi wa mpango. Ifuatayo ni baadhi ya mifano jinsi vikundi vimeweza kufanya kazi kwa mafanikio na viongozi wa dini na jamii kuongeza upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango.

Fanya kazi na viongozi wa dini. Baadhi ya watu hutumia mafundisho au maandiko ya kidini kujenga hoja kwamba uzazi wa mpango haustahili. Lakini dini nyingi duniani zinaunga mkono suala la kuzaa watoto kwa kuacha nafasi ya kutosha kati ya mtoto na mtoto, kwa sababu mpangilio huu hulinda afya na maisha ya wanawake na watoto. Hii ni kweli kwa watu wa imani tofauti, wakiwemo Waislamu na Wakatoliki.

Unaweza kuwaomba viongozi wa dini wanaotambua umuhimu wa uzazi wa mpango kulizingumzia suala hii katika jamii. Watu wanaposikia kuwa uzazi wa mpango hauendi kinyume na mafundisho yao ya kidini, hii inaweza kuleta unafuu mkubwa. Ni bora kutafuta njia za kufanya kazi ndani ya imani za watu za kidini ili chaguo lao la uzazi wa mpango liweze kuungwa mkono kutoka ndani kuliko kutarajia kubadili imani zao.

Oanisha uzazi wa mpango na utamaduni na mila za jamii husika

Jamii, hasa jamii za kikabila, zinaweza kutoziamini huduma za uzazi wa mpango kwa sababu baadhi ya programu huwashinikiza wanawake masikini kutumia njia za uzazi kadhaa au kufunga uzazi kabisa. Baadhi ya viongozi wa jamii za kikabila wanajitahidi kuingiza huduma za uzazi wa mpango katika huduma za afya za jamii zao kwa kuwashawishi wanawake kuchagua njia za kuzuia mimba ambazo wanaziafiki.

wanawake na watoto wakisubiri nje ya mlango wenye bandiko lenye maneno "Nyumba ya Afya."


Mfano mmoja ni kliniki nchini Ekueda (Ecuador) inayojulikana kama ‘Nyumba ya Afya’. Wafanyakazi wa afya kwenye kiliniki hiyo hutumia lugha ya asili ya eneo hilo, na wanaelewa na kuheshimu taratibu za tiba na imani za jamii hiyo. Kiliniki hiyo ina mganga wa tiba za jadi miongoni mwa wafanyakazi wake na pia bustani ya mimea/miti shamba. Duka la dawa hapo kiliniki hutoa aina zote 2 za dawa-dawa za kisasa na dawa za asili. ‘Nyumba ya Afya’ imejumuisha uzazi wa mpango miongoni wa huduma za kawaida ambazo zinatolewa kwa wanawake, watoto, na familia. Wenzi au wanandoa wameanza kuacha nafasi ya kutosha kati ya mtoto moja na mwingine kwa sababu za kiafya, na idadi ya vifo vya wanawake na watoto imepungua sana. Kwa sababu mila na desturi zinaheshimika sana, wanawake wanatumia huduma hizi kwa uaminifu.



Kujenga heshima na imani na viongozi wa jamii hufungua mijadala juu ya afya ya uzazi

Mradi wa Uendelezaji wa Mipango na Huduma za Afya kwa kuzingatia Mahitaji ya Kijamii (The Community-based Health Planning and Service project) nchini Ghana, Afrika Magharibi ulilenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya sehemu ya Navrongo, ambayo ni jamii ya kijiji kilichopo pembezoni chenye huduma duni. Katika kulifuatilia lengo hili, mradi ulifanya kazi kwa karibu na vikundi vya kijamii na kuleta wauguzi kutoka vituo vya afya maeneo ya mijini na sehemu za kati za wilaya kufanya kazi na jamii hiyo. Mradi uliandaa vikundi vya majadiliano vya marika ili wanakikundi wawe huru kuzungumzia masuala yao ya kiafya — vikundi vya vijana, wanaume wenye umri wa kati, wanawake vijana, wanawake wenye umri mkubwa zaidi, na viongozi wa jamii. Uzazi wa mpango ni miongoni mwa mada nyingi walizojadili.

HAW Ch7 Page 209-1.png

Walipoulizwa nini kifanyike ili huduma za uzazi wa mpango zitumike zaidi, wanawake walisema walitaka faragha zaidi katika utoaji wa huduma, na msaada katika kuwafanya wanaume kujisikia vizuri kuhusiana na huduma hizo. Wanaume walizungumzia juu ya heshima kuhusiana na watoto wengi, wasiwasi wa kupoteza mamlaka ndani ya nyumba zao iwapo hawatatakiwa kutoa idhini juu ya kuzaa mtoto mwingine, na kwamba mwanamke ambaye anatumia njia za uzazi wa mpango anaweza kumuacha mume wake.

Waendeshaji wa mradi walijifunza kwamba watu wanaweza kuwa katika hali ya kutumia zaidi huduma za uzazi wa mpango kama idadi ya vifo vya watoto kutokana na magonjwa itazidi kupungua. Hili tayari ndiyo lilikuwa lengo kuu la mradi huu wa afya. Na kadri wauguzi walivyoendelea kuwatibu wanaume kutokana na magonjwa yaliyokuwa yakiwasumbua, walianza kuwaamini na waliweza kuelezea njia za uzazi wa mpango mbalimbali na kujibu wasiwasi wa wanaume. Uhusiano ambao wauguzi walijenga na familia za jamii hiyo pia uliwasaidia kuingilia kati pale ulipotokea ugomvi kati wa wanaume na wanawake kutokana na matumizi ya uzazi wa mpango.

Mradi wa afya wa Navrongo ulitegemea sana ushiriki wa viongozi wa jamii — machifu, wazee, wakuu wa kaya, na viongozi wa vikundi vya kijamii. Heshima iliyojengeka ilisababisha machifu na wazee kuwa wanawakaribisha wawezeshaji wa mradi kuhudhuria mikutano ya kijamii, mahali ambapo masuala muhimu yanayohusu jamii hujadiliwa. Kwenye mikutano hiyo, wawezeshaji wa mradi waliweza kuelezea jinsi gani njia za kisasa za uzazi wa mpango zinaweza kuwasaidia wanaume katika hitaji lao la kijadi la kuachaa nafasi ya kutosha kati ya mtoto mmoja na mwingine. Na viongozi wengi kwenye jamii waliwambia wanaume wasigombane na wake zao wanaotumia njia za uzazi wa mpango.

Kupitia mikutano ya kijamii, mradi wa afya uliwezesha mijadala mingi zaidi juu ya afya. Mradi pia uliomba viongozi wa jamii kuwa wana waalika wanawake kuhudhuria mikutano ya kijamii, ambayo kawaida ilikuwa ni jukwaa la wanaume. Mwanzoni wanawake walikuwa na moyo mzito kuhudhuria, lakini mradi uliongeza ushiriki wao kwa kuvialika vikundi vya wanawake, kama vile kwaya au vikundi vya kidini, vikundi vya kiuchumi na mitandao ya kisiasa. Hii iliwezesha wanawake pia kushiriki katika mijadala mingine ya kijamii.